Ripoti ya Mwisho

Mtazamo katika maisha yangu huko Tanzania

 

16/10/2012

 

Zaidi ya mwaka moja nyuma niliposhuka Dar es Salaam katika hilo joto sikukufikiria vitanitokea vitu gani. Japokuwa tulizungumzia vitu vingi katika muda wa kujiandaa sikupata picha kwa ujumla. Katika hizo wiki mbili za semina ya KAWAIDA e.V. Hamburg voluntia wenzangu David na Chris na mimi tulijifunza vitu vingi kuhusiana na Tanzania, Utamaduni wake, ubaguzi, kufanya kazi na watoto na kiasi kidogo cha Kiswahili. Tulipata matumishi binafsi na semina ilikuwa katika hali njema kwa sababu tulikuwa voluntia watatu tu. Hata niliweza kumuona Alfred antakayekuwa mkurugenzi wangu na menta wetu. Alikuwa anaongea sana kuhusu utamaduni wa Tanzania na nilikuwa na tabu kuelewa kiingereza chake lakini ilikuwa vizuri kumsikiliza mtanzania. Katika hii semina nilijifunza vitu ambavyo nilijua vitanisaidia katika kazi na maisha huko Tanzania.

Hata kama uwoga wangu ukazidi, nilitaka kuwahi kufika Tanzania na kuona nilichosikia sana. Nilikuwa na hamu sana ya kufika Tanzania.

 

Nilipokuwa kwenye ndege nilikuwa mwoga sana lakini niliposhuka na kuona voluntia wengine waliotutangulia sikuogopa tena. Uwoga haujarudi tena. Nilipokaa kwenye teksi ya kwenda nyumbani na kupita Nelson Mandela Road mara ya kwanza kabisa nilikuwa nashangaa tu. Sijakuwa hata na muda wa kufikiria uwoga wangu. Kuangalia dirishani kwa teksi ilikuwa inatosha kunishihiri.

 

Nilijuwa vitanitokea hata vitu vibaya katika utamaduni, kuibiwa au kwamba hawatanipenda kwa sababu mi mgeni lakini baada ya muda mfupi niliona kwamba watu wapo wazuri na kwamba wanapenda wazungu. Walikuwa wananiheshimu sana. Mwanzoni heshima yao ilinitoa uwoga wangu lakini baadaye ikaanza kunisumbua kwamba wananiona tofauti. Kiukweli nimepokelewa vizuri sana na watanzania!

 

Kabla ya kuondoka Ujerumani nilijuwa nilijifunza Kiswahili na nitaweza kuongea angalau kidogo lakini nilipofika sikuelewa hata neno na suala hilo likanisumbua. Nikapata changamoto nyingi na nilianza kujifunza lugha hilo kwa bidii na furaha. Tena watu wengi walipenda kunisaidia wa kwanza waalimu wa TSE. Ndio maana nikaendelea haraka. Sasa hivi naongea bila wasiwasi.

 

Nilipoona sehemu yangu ya kufanyia kazi Talent Search and Empowerment (TSE) mara ya kwanza kabisa nilikuwa nashangaa sana kwamba mahali ni padogo – vyumba viwili ambavyo vimejaa hadi juu na ua kwa nyuma. TSE ni kituo cha vijana cha kujifunzia maigizo, kuimba, kucheza, ngoma, Hip Hop, kupiga gitaa, kompyuta nk. Waalimu wao ni vijana wanaokaa karibu na mimi na umri wananizidi kidogo tu. Mwanzoni walinisaidia sana na halafu wakawa marafiki zangu. Wakanipokea kwa wema na walikuwa wenzangu na wakati moja waalimu wangu wakuu kwa kiswahili.

 

Mwanzoni sikuwa na kazi kwa sababu sikuweza kuendeleza masomo ya kinanda na gitaa ya Thurid aliyenitangulia kwa sababu sijaweza kupiga chombo fulani. Kwa hiyo nikatafute kazi zangu mwenyewe kisha nikajaribu vitu vingi sana. Nilipenda sana kubuni. Kuna siku nilijaribu kufundisha mahesabu, kufanisha kazi za ofisi, kuchezea parashuti ya kutoka ujerumani au nilifunga kamba ya kutembea katika miti miwili uani. Siku zingine nilichora na wadogo au nilicheza nao au kufundisha kompyuta siku nzima. Baada ya muda mfupi tu nilikuwa na mambo mengi.

 

Kila mwezi kazi yangu ofisini ilikuwa kutafsiri ripoti za waalimu za kiswahili kwa kiingereza na kutuma Ujerumani kupitia E-Mail. Zaidi ya hayo nilipaswa kupokea michango kutoka Kigogo, kutafuta risiti zote, kuandika ripoti na maombi ya kupata hela zingine. Thurid alikuwa amenifundisha lakini hata hivyo mwanzoni ilikuwa ngumu sana kwangu. Nilijiuliza kwa nini mimi nifanye kazi hio wakati mimi ni mgeni sana? Watu wote wananiamini kwa sababu mi mzungu na watu wa zamani sio waaminifu? Baada ya muda nilipata uzoefu na confidence.

Lakini kiukweli kazi hio ni ngumu sana kwa mgeni. Paula anayenifuata nilimzuia kufanya kazi hio. Mchanga wa Dogodogo-Centre nikatoa wote na nikamalizia nao ili Paula aweze kuanza na mkataba wake na aelewe kila kitu akiwa amezoea Tanzania kidogo.

 

Halafu nikaanza kufundisha sarakasi kila ijumaa baada ya wiki mbili. Watoto walipenda lakini kufundisha ilikuwa mgumu kidogo kwa sababu ua una uchafu mwingi, chupa na vumbi nyingi yaani haifai kabisa. Lakini hata hivyo nilikuwa nafundisha. Hata kama watoto wengine walikuwa hawataki kunitii wote walifurahi ndani yake mimi mwenyewe. Ningependa watoto walewale wangekuja kila somo la sarakasi na sio kila mara wengine. Ningeweza kuwaendeleza na kuwafundisha. Hivi niliwafundisha sarakasi moja moja na walijua wengine na wale ambao hawataki hawajajifunza vizuri. Zaidi ilikuwa kuwafurahisha na sio kuwafundisha.

 

Katika siku zangu za mwanzo nilinunua nyuzi za kuwafundisha watoto wangu kushonea bangili. Kwa sababu walipenda kalcha, hizo nyuzi zilikuwa chanzo cha mradi wa kalcha. Nikaomba fedha kwa Kawaida na nikanunua nyuzi zingine, shanga nk. kwa ajili ya kutengenezea mikufu, bangili na hereni zilizouzwa. Bahati mbaya zikapotea kalcha nyingi kabla hatujaweza kuuza. Katika wakati ambayo mimi sipo zikapotea zaidi. Japo tukaingiza hela ndogo ya kununua vifaa vya kuendeleza huu mradi. Natumaini kwa sasa Paula anauendeleza huo mradi.

 

Mradi wangu mkubwa wa pili ulikuwa mradi wa kuchora. Mimi mwenyewe napenda sana kuchora ndio maana ninafikiri kipaji hicho nikakiingizie na nifundishe watoto kuchora. Pamoja na Chogo, msanii mwenzangu na Teacher Morsi tukaenda mjini kununua vifaa na kuwafundisha watoto kutengeneza fremu za kuchorea kuzivalisha vitambaa kupaka kozi na kisha kuchora. Nilikuwa nabunibuni na mara nyinigi ikawa ovyoovyo lakini mwishoni zikatoka picha nzuri na wote walifurahi na kujifunza vingi hata mimi. Napenda kama mradi huu unaendelea. Labda Roger, mwanafunzi wa TSE anaweza akaendeleza huo mradi kwa sababu yeye ameelewa kila kitu.

 

Miezi mitano ya mwisho mara mbili kwa wiki moja nilifundisha Kijerumani. Hapa nilikuwa na tatizo kwamba watoto hawakuji kila mara wengine walipotea madaftari yao na mara nyingine hawasikilizi kwa umakini nilivyowaomba. Wanafunzi watatu walishika vitu fulani na wengine nina wasiwasi nao. Lakini Paula anaendeleza masomo yangu. Sasa nafurahi kwa sababu labda hawatasahau kila kitu.

 

Mara nilitaka kupanda alizeti katika dumu za maji. Mwanafunzi wangu Erick alinisaidia na bidii. Mwanzoni watu walinishangaa lakini maua yetu yalipoota vizuri tukajidai nayo. Alizeti zilipoota kubwa nilizihamisha kwenye ardhi. Huko ziliendelea kuota vizuri na zenye afya lakini baada ya muda mfupi zimeng’olewana wapita njia. Sikupenda lakini nifanyeje?

 

Kazi yangu nyingine ilikuwa kumiliki ziara za TSE yaani kudili mambo ya hela, kutafuta gari na dereva, kuandika barua za wazazi na kujadili na wahusika. Mwanzoni niliogopa kazi hio lakini hata hivyo kila kitu kikafanyikiwa. Ziara za beach na sehemu zingine nilienjoy sana. Na pia nadhani ni muhimu sana kwa watoto waone sehemu mbalimbali.

 

Kitu kingine kinachofanyikiwa kilikuwa Watoto Talent Show, mashindano katika nanja dance, mziki na maigizo. Japo hatujaweza kufuata mipango yetu yote kwa mfano majaji wa maigizo hawakuji bila taarifa, maiki zililia vibaya na Baba Watoto walichelewa sana. Lakini hata hivyo watu walinisifia sana na watazamaji walikuja wengi. TSE ikashinda vitu vingi kwa sababu wanafunzi wetu ndio walipata taarifa zote mapema. Sasa je, mnaweza kuendeleza na Watoto Talent au imekuwaje sasa? Tumejifunza vitu vingi na mara ya pili itakuwa iko poa zaidi.

 

Halafu tuliweza kurekodi wimbo uliotungwa na Erick na kushuti video yake. Majukumu yangu yalikuwa mambo ya fedha, kusindikiza watoto wangu kila sehemu na kuongea na maproducers. Hamis, mwenzangu wa TSE anayedili mambo ya production ya video alikuwa mshika kamera na cutter. Nilipenda kuangalia alivyofanya kazi na nilijifunza vitu vingi. Kiukweli yeye ni mtaalamu na anaweza kazi yake. Niliwasikiliza watoto na wengine hawajarithika na video na wakasema Hamis hawasikilizi vizuri. Lakini naona ni muhimu kuwasikiliza watoto wakati ni video yao!

Kinachonisikitisha ni kwamba sijawahi kuona video ambayo imetimia… Siku hio ya kumalizia kuedit hard disc yake Hamis ikashindwa kutumiwa tena kwa ajili ya virus fulani. Video, tuliyokuwa na kazi nyingi sana imesemwa kupotea. Siku za kushuti video zilikuwa vizuri nilizipenda na nilikuwa na hamu ya kuangalia video na sasa imepotea… Inanisumbua yaani sipendi kabisa lakini siwezi kufanya kitu. Au mmeweza kutengeneza hard disc sasa? Kiukweli inaniumiza sana.

 

Kuelekea mwishoni wa muda wangu Madam Haika aliniongeza taabu katika kazi yangu. Alikuwa kama hana bidii tena, na alijaribu kuondoka mapema na kuelekea nyumbani, hata kama mwaka huu aliweza kuwahi kuondoka saa moja kulinganisha na mwaka uliopita. Alipendelea kwenda mjini kuliko kuja TSE. Alikuwa kama mtu anayechoka kazi. Mara nyingi asubuhi nilipata SMS yake kwamba anachelewa ofisini na nikafungue mimi. Siku nyingi nikaanza siku zangu za kazi saa moja na nusu ili wanafunzi wa kompyuta wasisubiri mlangoni kwa muda mwingi. Sio kazi ya voluntia kufungua na kuwafundisha wanafunzi wa kompyuta peke yake…

Nikapata majukumu mengi na Morsi aliwahi kusema „TSE ndio ni ofisi ya Franzi sasa.“ na kama nilikuwa sipo siku moja na mtu akafika alinipigia simu hata kama angeweza kumuliza mtu mwingine kuhusu suala hilo. Haina shida kwa sababu nilikuwa nimeshachangamka wakati huo na nimezoea lakini msingeweza kuanza na Paula hivyo hivyo.

 

Kitu kimoja ambacho sijamsamehe madam ni kwamba ametufungia nje siku moja bila kututolea taarifa kwamba anaondoka. Begi langu na ufunguo wa ofisi, simu yangu na simu ya Aisha na ufunguo wa chumba cha Aisha na hata viatu vyangu vilifungiwa ndani. Alikuwa amepigiwa simu sana na sisi lakini hakupokea kabla hajafika nyumbani kwake. Mbezi ni mbali na tulishindwa kumfuata hadi kule. Ndio maana nikarudi nyumbani pekupeku na Aisha kalala kwetu. Sio tabia nzuri na nikakasirika kweli. Tena alijifanya kama amekosea kufunga bila kutuambia lakini sidhani kwamba mtu anaweza akasahau kuaga kabisa. Sema yeye ndio hawezi akapata tabu na tena mkurugenzi anamtetea. Aisha na mimi tulijisikia kama hatuna haki.

 

Mwanzoni Alfred na mimi hatujaelewana. Yeye alikuwa boss wangu na ana nguvu na anaweza akaamua, mara nyingi alikuwa yuko bize sana kwa sababu ana kazi nyingi sio TSE peke yake lakini alitaka taarifa za vitu vyote. Hata waalimu wengine walijisikia hivyo. Na pia mimi sikutaka kumsikiliza yaani sikupenda kumuambia kila kitu kwa sababu niliogopa atanizuia.

Katika semina ndogo cha sisi voluntia watatu na Alfred alitusomea menta aweje lakini hakufikiria kama yeye yuko hivyo. Cha kwanza ilinisumbua sentence moja vile: „Menta asiwe kama boss, awe rafiki wa voluntia ili kwa mfano aweze kumpigia simu hata usiku akiwa na matatizo.“

Ikanisumbua kwamba nilishindwa kumuambia kwamba sio hivyo kabisa na kama ni vile hawezi akawa menta. Bora voluntia wanaotufuata waweze wakachagua wenyewe menta wao ni nani. Boss na menta ni nyingi kwa mtu moja, ni kitu ambacho hakiwezekani. Ndio maana Alfred alikuwa mkurugenzi wangu sikumuona kama menta yangu. Kuhusu matatizo yangu binafsi niliongea na Mama Lina, waalimu wenzangu au KAWAIDA.

Kuelekea mwishoni kwa kipindi changu nikaanza kuelewana na Alfred. Tuakaanza kufanya kazi vizuri kwa pamoja na hatujagombana tena. Nilijuwa kwamba kila kitu nimuambie kwanza na nimulize kama ni sawa, mara zote ikawa vizuri. Tukasaidiana hivyo ndivyo ilinirahisisha kazi yangu sana. Alikuwa amenisifia kwamba nafanya kazi vizuri na kwamba napenda kazi. Ningependa hata mapema iwe hivyo.

 

Lakini japo yale matatizo, TSE kama sehemu ya kufanyia kazi kama voluntia imekomaa. Niliweza kujaribu kila kitu, hakuna mtu aliyeweza au aliyetaka kunizuia kitu na waliniacha nijaribu tu. Tena ni sehemu nzuri sana kujifunza utamaduni wa kitanzania, kuongea kiswahili na kupata marafiki wazuri ambao wamenisaidia sana kuniingiza katika jamii. Tena kama voluntia anataka kubuni TSE ni pazuri. Tatizo moja ni sehemu ya kufanyia mazoezi ni ndogo sana na sasa tena Anse kajenga baa yake na ikapunguza tena sehemu ya mazoezi.

 

 

Kwa kila siku nikafanya kazi muda mrefu kuliko „weltwärts“ waliniruhusu. Siku nzima nilikuwa TSE na muda wote nilikuwa bize, lakini huko ndio walikuwa marafiki zangu. Muda mwingine sikuongea kijerumani, ila nikifundisha TSE. Labda msimfanyishe voluntia kazi muda wa siku nzima kama anachoka haraka. Kwanza hairuhusiwi halafu sio vizuri kama anachoka sana kazi. Pendekezo langu ni kama amefanya kazi zaidi ya masaa nane kwa siku (kwa ujumla masaa arobaini kwa wiki) apate luksa asubuhi moja moja ili aweze kulala, kupumzika au kufanya anachotaka.

 

Ndio nilikaa na David lakini saa zingine tulikuwa tuko bize mpaka hatuonani.

Lakini sio kwamba hatujakuwa na nafasi ya kufanya vitu binafsi. Usiku baada ya TSE nilienda Baba Watoto-Centre kwa ajili kufanya mazoezi ya sarakasi. Nilimjua mwanasarakasi anayependa kunifanisha mazoezi usiku. Nilipenda sana kufanya mazoezi naye japokuwa mara nyingi tulifanya mazoezi kwenye giza umeme ulikuwa umekatika.

Karate nikaacha baada nusu mwaka kwa sababu njia ilikuwa ndefu sana, sikupenda sana kupigiana na mara nyingi nilikuwa niondoke mapema kidogo TSE na sikupenda kama sikuweza kuangalia mazoezi ya waalimu wengine hadi mwisho.

 

Katika wikiendi nilisafiri, nilienda kwa concerts na kwenye mashoo, nilitembelea marafiki zangu, nilienda kushona ushonaji wa TSE, nilialikwa kwa masherehe, nilichora pamoja na Chogo, nilienda baharini, mjini nk.

Sikuwahi kuboreka hata sekunde.

 

Na pia sehemu ya kukaa kwa Mrema imekomaa. Tulikaa wawili katika nusu ya nyumba nzuri sana. Nusu nyingine wanakaa Mama Lina, Mary, Shedy na Mamake. Nawapenda sana na nawashukuru sana kwa sababu wasingekuwa watu wazuri nisingependa kuja nyumbani nilivyopenda. Mama Lina alikuwa kama mamangu. Nilipokuwa na matatizo, na njaa au kama nilitaka kuwa na watu au kama niliumwa niliweza kwenda kwao na walikuwepo. Ndio maana muda wote nilipofika nyumbani sikuwa upweke lakini kama nilitaka kupumzika peke yangu niliweza kufunga mlango.

 

Nilikuwa siangaiki na matatizo kwa hiyo niliweza kufanya kazi vizuri TSE na kujifunza vitu vyingi vya kiutamaduni.

Kitu kilichokuwa kizuri kuliko vyote ni kujifunza Kiswahili na kupata marafiki wa karibu ambao wamekuwa watu muhimu sana kwangu. Ndio maana nikapata tabu kuwaaga na kuzoea tena Ujerumani. Sherehe yangu ya kuniaga na kuniaga kwenye wanja wa ndege zilikuwa vizuri sana lakini pia ya kusikitisha. Nililia sana na ikauma sana kwa sababu sijui nitaweza kurudi lini ila najua lazima nirudi siku moja.

Kufika Ujerumani ilikuwa vizuri sana na ilifanana na siku ya kwanza kufika Tanzania japokuwa Ujerumani niliwahi kuishi miaka mingi tayari na niliwahi kupaona. Nilipokelewa vizuri. Nilipenda kuwaonana na marafiki zangu wa zamani na kuwaadithia Tanzania ikoje.

Sema wengine wananisumbua. Wengi wananiuliza. „Vipi ilikuwaje?“ lakini kama naanza kuwaadithia baada ya dakika tano hawanisikilizi tena… Lakini siwezi kufupisha mwaka mzima uwe dakika tano. Haiwezekani kabisa… Kwa hiyo mara nyingi na jibu „vizuri“ basi na siulizwi tena. Watu hawanielewi na hawawezi kupata picha ndio maana wanaendela kuchekacheka tu. Mara nyingine nawachoka nawaona kama watoto ambao hawajui chochote cha dunia.

 

Semina ya mwisho ilikuwa vizuri hata kama ilikuwa mapema mno baada ya wiki moja ya kushuka Ujerumani. Mada nyingine ningependa kuzifikiria kwanza lakini nilikuwa sijapata muda bado. Ilikuwa vizuri kwamba niliweza kuongea na volunteer wengine kutoka South Africa na wengine Ghana.

Watu wakiwa waliwahi kufanya kazi nchi nyingine wanapenda kunisikiliza zaidi ya dakika tano. Wanafananisha kazi zao na kazi zangu na wanaweza kunielewa kwa sababu waliona vitu ambavyo vinafanana.

 

Nadhani katika muda huo Tanzania nimebadilika. Nimejifunza kuwa na majukumu makubwa, niliona na kusikia watu wengi katika duniani wanavyoishi, nilijisikia huru sana, nilijifunza lugha nyingine na watu wa utamaduni mwingine nimewazoea. Siogopi tena kucheza na kuimba, nimepata marafiki wapya, na nimezoea vitu fulani ambavyo havipo Ujerumani. Nimekuwa mvumilifu na sitoboreka tena katika maisha yangu. Nimeona kwamba naweza kuishi na kufurahia sehemu yoyote.

 

Tanzania imekuwa nyumbani kwangu na siku nyingine lazima nikasafiri tena kwa sababu naumia. Nitaendelea kuwasiliana na Aisha na Oliver na pia watu wengine ambao nilikuwa nao katika muda huo. Sitowasahau watu wala Tanzania kwa ujumla. Hata tutaendelea kushirikiana hata kama niko mbali kidogo tuko pamoja. Halafu hapa ujerumani kuna baridi sana wakati msimu wa baridi haujaanza bado. Natamani nikimbie!

 

Kwenda Tanzania – nadhani ilikuwa uchaguo bora, nina uhakika imenisaidia sana na sitoweza kukiacha kila kitu nyuma yangu. Ilikuwa nzuri! Sio kwamba nauongopea nikijibu vile kama naulizwa „Vipi ilikuwaje?“

 

Nawashukuru sana kwa kunipokea kwa wema na kunilea, kunilinda na kunifundisha kiswahili mpaka nimekuwa kama mtanzania. Sasa naweza nikaishi kwenu na nitarudi baada muda. Kwa sasa sijaanza kusoma lakini nimeamua nataka kusoma masomo gani. Nitasoma mambo ya kulea na kufundisha pamoja na media, sanaa au utamaduni. Nikishamaliza kusoma nitaweza hata kufanya kazi Tanzania. Na sio kazi ya kubunibuni tena nitakuwa mtaalamu wa kitu fulani.

 

Kwa sasa kila Jumanne nafundisha wasichana wa darasa la kwanza sarakasi. Wako watundu kumi na nne na wananiangaisha sana. Lakini nawapenda na wananipa changamoto. Tena sarakasi naipenda sana.

Wiki hii nitaenda kufanya mazoezi ya sarakasi chuoni. Natumaini itakuwa vizuri.

Halafu baada ya wiki mbili nitaanza kufanya kazi kwenye kituo cha watoto kama TSE lakini cha kijerumani. Nitafanya kazi ya kujitolea kwa muda wa mwezi moja.

 

Nawaomba niye muendeleze TSE na kazi zenu ili nitakaporudi nikute TSE ikasonga mbele.

Tutaonana!

 

Franziska Müller, Freiwillige Kawaida e.V.