Ripoti ya Franziska ya Mwaka mmoja - Kazi yangu huko TSE

03/07/2012

 

 

Kazi yangu hapa TSE nimeanza mwezi wa nane mwaka uliopita. Kwanza niliangalia sana mazoezi ya waalimu wenzangu, kujifunza kiswahili, kucheza na watoto wadogo na kuanza kufikiri vitu vya kufundisha. Wiki ya kwanza nilianza kufundisha kompyuta na kuwafundisha watoto wadogo kuandika na kuhesabu. Halafu nilifunga kamba katika miti miwili na kuwafundisha watoto kutembea juu ya kamba. Baada ya muda nilianza kufunga kamba kila siku kwa saa moja na kwa sasa wanafunzi wangu wengine wanajua kutembea kwenye kamba vizuri. Na pia nilifika na parashuti ya kucheza na watoto walifurahia sana.

Kitu cha pili nilichoanzisha hapa TSE ni kutengeneza kalcha. Mwanzoni kabisa nilianza kuchukua nyuzi na kushona bangili. Ilitokea wazo la kuuza zile kalcha. Tulianza kutengeneza na kalcha za shanga na kuvaa shingoni na hereni. Sasa hivi tunapata oda na tunawatengenezea wateja. Watoto wengi wanajua tayari kutengeneza vizuri. Lakini tuna matatizo kama kwa mfano kacha nyingi zinapotea na pia vifaa vinapotea na kalcha nilizozipeleka kwenye ofisi ya ushonaji ya TSE hazinunuliwi.

Katika miezi ya kwanza tulikuwa na mashoo mashuleni. Huko ndio tulitangaza TSE ili watoto wa shule wajue kwamba kuna sehemu ya kujifunza vitu wanavyoviona. Na kweli idadi ya watoto ikaongezeka. Mimi mwenyewe nilitangaza mchezo mpya ya kutembea kwenye kamba.

Mradi wangu wengine ni mradi wa uchoraji. Mimi mwenyewe napenda kuchora na nimeamua kufundisha wanafunzi wangu. Kwanza tulikuwa na rangi za maji. Tulichora kwenye karatasi siku moja moja mpaka rangi ziliisha. Halafu nilipanga kuwafundisha kuchora kiutalaamu kwenye fremu za kuchorea. Kwanza nilifanya mazoezi nao ya kuchora na penseli na rangi kwenye karatasi. Halafu niliomba fedha kutoka kwa KAWAIDA na nilianza kununua vifaa vyote. Mwanzoni tuliwafundisha kukata mbao, kugonga misumali ili mwishoni wanajua kutengeneza fremu na kuivalisha kitambaa na kupaka kozi. Nilifundisha uchoradi katika kila kipindi cha pili cha Teacher Mors kwa hiyo ulichelewa sana. Kwa hiyo tulipanga wiki moja kwa ajili ya uchoraji tu. Mazoezi yote mengine walipunzika katika wiki hii, tulichora sana na zimetokea picha nzuri sana.

Wazo lingine lilikuwa kufundisha sarakasi. Kila ijumaa kama kikao hakipo nafundisha sarakasi ila sio rahisi katika sehemu yetu ya mazoezi. Chini kuna mawe, uchafu na machupa na unaweza ukaumia sana ukikanyaga vibaya. Taratibu taratibu watoto walijua kidogo lakini sio sana. Kipindi hiki nashirikiana na Mors katika masomo yake ya Hip Hop. Aliniomba nimsaidie kuingiza sarakasi kwenye dansi.

Siku moja nilikuwa na wazo la kupanda alizeti. Ziliota vizuri na mimi na watoto tulizitunza sana lakini siku moja tulikuta hazipo tena zimeng’olewa na wapiti njia.

Siku nyingine niliwahi kufundisha mahesabu.

Halafu namsaidia Madam Haika kushinda na miradi midogo ya ofisi kama kuuza maji, kuchapa kazi za kiofisi kama zipo na kuprint. Na pia mara kwa mara nafundisha kompyuta. Katika vipindi viwili vya likizo za Madam Teacher Aisha na mimi tulikuwa na majukumu ya kufundisha kompyuta peke yetu.

Jukumu langu lingine ni kuomba na kutunza fedha kutoka KAWAIDA na kwa Bernhard Staub. Kwa upande wa hela kutoka kwa KAWAIDA niandike maombi ili natumiwa zile hela. Nizitunze na nisanye risiti zote na kuzirudisha. Katika upande wa mchango kutoka kwa Bernhard Staub niandike vile vile maombi na nipeleke Kigogo. Huko wanaiangalia na siku nyingine niende tena kwa ajili ya kupokea hizo pesa. Baada ya kutumia nirudishe repoti yake na risiti zote. Mwanzoni niliogopa ile kazi ya fedha kwa sababu niliona ni jukumu kubwa sana na naweza kukosea na kuharibu vitu vikubwa.

Ile michango ilituwezesha ziara nyingi ya kutembelea Baba Watoto Centre, Dogo Dogo Centre na safari za kwenda beach. Huko ndo tulifanya mazoezi pamoja na vile vikundi vingine na katika mazingira tofauti. Watoto, waalimu na mimi mwenyewe tulifurahi sana katika siku hizo.

Pia zile hela zilikusaidia sana kununua vifaa vya mazoezi kama maspika, matumizi ya stationary, ngoma, mavazi ya shoo nk.

Pamoja na mwalimu mwenzangu Aisha niliwahi kutembelea wazazi au walezi wa wanafunzi wetu ili tujue wanavyoishi na tuwaambie wazazi watoto wao maendeleo yao hapa TSE. Ripoti tukapeleka ofisini kwa mkurugenzi wetu.

Katika miezi minne nafundisha kijerumani. Nafurahi kwa sababu wanafunzi wangu wanaanza kunielewa na naona maendeleo. Lakini wengine hawaji siku moja moja na wanakosa mafunzo. Na siku nyingine hawana hamu ya kufundishwa. Maranyingi nawaita waje kusoma lakini wanakaa tu na kuwafokea sipendi.

Kazi yangu ya kila mwezi kuanzia mwanzo ni kutafsiri ripoti za waalimu wa sanaa. Natafsiri maadishi yao ya kiswahili kwa kiingereza na kuwatumia KAWAIDA.

Hata sasa hivi bado napenda kuangalia mafunzo ya waalimu wenzangu ya maigizo, mazoezi ya viungo, Hip Hop na sarakasi, ngoma na mziki. Mara nyingine na shiriki kama mwanafuni mara nyingine nasaidia waalimu, nawashauri na kutoa mawazo.

Mwezi wa sita tulikuwa na tamasha letu la hapa TSE linaloitwa WATOTO TALENT SHOW. Tulibuni hilo wazo kwa pamoja, tuliliendeleza na kuandaa. WTS ni mashindano katika nanja tofauti kama ngoma za asili, maigizo na mziki. Tulifanikiwa hata kama haijakomaa kabisa. Katika talent show itakayofuata mwezi wa nane tutajaribu kuboresha na kutoa yale makosa ambayo yaliyojitokeza na mapungufu.

Sasa hivi tuko katika harakati ya kurekodi nyimbo moja ya watoto. Tutawapeleka kwenye studio na baada ya kumaliza kutengeneza audio tutatengeneza na video.

 

Franziska Mueller, voluntia wa TSE